Hii ni blog ambayo inakupa Taarifa na habari Zote Za Kitaifa na za kimataifa Katika Nyanja Zote za kisiasa, Uchumi, michezo na burudani..

Wednesday, April 9, 2025

Lissu akamwatwa na jeshi la Polisi Mbinga

 Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu amekamatwa na Jeshi la Polisi Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo amekamatwa wakati alipomaliza mkutano wa hadhara uliofanyika leo April 09, 2025 katika Jimbo la Mbinga na taarifa iliyotolewa na CHADEMA imesema mpaka sasa haijulikani Lissu amepelekwa kituo gani cha Polisi. 


Lissu amekamatwa pamoja na Wanachama wengine akiwemo Aden Mayala , Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Felius Festo , Mratibu wa Uhamasishaji BAVICHA Taifa, Shija Shebeshi  na Mlinzi ambapo CHADEMA imelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia Viongozi hao haraka na bila masharti yoyote.


CHADEMA imesema wakati wa zoezi la kumkamata Lissu, Wananchi wametawanywa kwa mabomu uwanjani na Polisi wametumia pia risasi za moto na kupelekea baadhi ya Wananchi kuumizwa. (video imerekodiwa muda mfupi kabla ya Lissu kukamatwa).



Jitihada za kulitafuta Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma ili kupata taarifa zaidi zinaendelea. 

Tuesday, April 8, 2025

 WANACHAMA 200 WA ACT WAZALENDO WAJIUNGA CCM

Wanachama 200 wa Chama cha ACT Wazalendo, wakiwemo viongozi wa ngazi za juu kama Katibu wa Chama hicho Jimbo la Tunduru Kusini, mkoani Ruvuma Saidi Mponda, na Diwani wa Kata ya Mchoteka, Sefu Hassan Dauda, wamejiunga rasmi na Chama cha Mapinduzi (CCM).



Uamuzi wao wa kuhama ACT Wazalendo na kujiunga na CCM umetokana na kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 


Wanachama hao wamesema kuwa Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuboresha sekta za miundombinu, afya, elimu, na uchumi kwa ujumla.



Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mlimgoti, wilayani Tunduru, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewapongeza wanachama hao kwa uamuzi wao wa kujiunga na CCM. 


Amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye misingi ya maendeleo na akatoa wito kwa wanachama wa vyama vingine kujiunga na chama hicho ili kushirikiana katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.



Aidha, Dkt. Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu dhamira ya CCM kuendelea kusimamia maendeleo na kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na rasilimali za nchi. 


Amesema kuwa Serikali inayoongozwa na CCM itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.


Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa Watanzania wote kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote, akisisitiza kuwa mshikamano wa kitaifa ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu.

Tuesday, April 1, 2025

Kapteni Ibrahim Traore Rais na Kiongozi wa jeshi la Burkina Faso, ametoa msamaha kwa wanajeshi 21 waliohusika katika mapinduzi ya serikali ya Septemba 2015.


Katika amri iliyotiwa saini Machi 24 Kapteni Traore aliweka masharti ya msamaha, ambao ulipigiwa kura mnamo Desemba iliyopita na bunge la mpito.


Wanajeshi hao 21, wakiwemo maafisa, maafisa wasio na kamisheni na vyeo vingine, walifikishwa mahakamani au kutiwa hatiani kwa matendo yaliyofanywa Septemba 15 na 16, 2015, inasema amri iliyotiwa saini na Kapteni Ibrahim Traore.


Hata hivyo, amri hiyo inaeleza kuwa kurejeshwa kazini kufuatia msamaha hakuwezi kutoa mwanya wa urekebishaji wa kazi au fidia.


Kutiwa saini kwa amri hii kunafuatia kupitishwa mwishoni mwa Desemba 2024, na bunge la mpito, kwa sheria ya msamaha na masharti ya kutoa msamaha kwa watu waliopatikana na hatia kuhusiana na mapinduzi yaliyofeli ya 2015.



Sheria hii inabainisha kwamba askari waliotiwa hatiani au kufunguliwa mashtaka kuhusiana na kesi hii, na wanaoonyesha kujitolea katika mapambano dhidi ya ugaidi, wanaweza kuchukua fursa ya neema ya msamaha ili kupandishwa cheo katika kazi zao. 

Friday, March 21, 2025

 Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Moshi Jonathan Kabengwe, amesema majina ya Waombaji wa ajira 1,596 zilizotangazwa na TRA hivi karibuni yatatangazwa rasmi kesho March 22 2025 kupitia tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) kwa ajili ya usaili wa kuandika utakaofanyika March 29 na 30 mwaka huu kwenye Vituo 9 tofauti vya Tanzania bara na Visiwani.




Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam leo tarehe 21.03.2025, Kabengwe amesema kati ya Waombaji 135,027 waliotuma maombi ya nafasi hizo za ajira, Waombaji 112,952 wamekidhi vigezo na kuitwa kwenye usaili wa kuandika ambapo sasa kila Muombaji atatumiwa katika barua pepe yake taarifa ya kuitwa kwenye usaili ambapo pia Waombaji wenye mahitaji maalum watawekewa utaratibu maalum ambao utawasaidia kufanya usaili bila usumbufu.


Kabengwe amesisitiza kuwa Waombaji wote watatendewa haki na kwamba usaili huo utafanyika kwenye Mikoa 8 ya Tanzania Bara na kwa Visiwani Zanzibar usaili utafanyika Unguja na Pemba kama inavyoonekana kwenye orodha ifuatayo.


1. Dar es salaam ambayo itahusisha Waombaji kutoka Dar es salaam na Pwani.


2. Zanzibar ambayo itahusisha Waombaji kutoka Unguja na Pemba


3. Arusha ambayo itahusisha Waombaji kutoka Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.


4. Dodoma ambayo itahusisha Waombaji kutoka Morogoro, Dodoma, Singida, Iringa na Tabora


5. Mtwara ambayo itahusisha Waombaji kutoka Mtwara, Lindi na Ruvuma


6. Mbeya ambayo itahusisha Waombaji kutoka Mbeya, Songwe na Rukwa


7. Mwanza ambayo itahusisha Waombaji kutoka Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu.


8. Kagera ambayo itahusisha Waombaji kutoka Kagera na Geita.


9. Kigoma ambayo itahusisha Waombaji kutoka Kigoma na Katavi.

Thursday, October 17, 2024

 Klabu ya Pamba Jiji Fc imethibitisha kumteua kocha Fred Felix 'Minziro' kuwa Kocha Mkuu akichukua mikoba ya Goran Kopunovic aliyetupiwa virago Oktoba 16, 2024.


Taarifa ya leo Oktoba 17, 2024 iliyotolewa na Kaimu C.E.Ο kwa klabu hiyo, Ezekiel Ntibikeha imebainisha kuwa Minziro atashirikiana na Kocha msaidizi Mathias Wandiba.


“Uongozi wa Pamba Jiji Fc unawatakia kila la kheri katika kipindi hiki cha kazi yao mpya, huku wanamwanza wakiwa na matumaini kibao ya kuiona Pamba Jiji ikifanya vizuri Ligi Kuu.” — imesema taarifa hiyo.

Wednesday, October 16, 2024

 Kamanda wa Polisi Jamii Wilaya ya Kipolisi Ukonga ASP Novatus Edmund Mallya amewaasa Polisi Jamii kuacha kutumia vibaya mwamvuli huo katika kutekeleza majukumu yao pamoja na ndani ya jamii wanayoishi.



ASP Mallya ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa Wananchi ndani ya Wilaya hiyo, "Tunapata malalamiko kutoka kwa Wananchi kuwa mnafanya matukio ya ajabu na ubabe kisa tu ninyi ni Polisi Jamii, hii sio sawa acheni kukamata Watu bila kufuata utaratibu mzuri , Biashara haramu na matendo mengine yanayokinzana na sheria za nchi ninyi muwe mfano hakuna aliye juu ya sheria."



Monday, October 14, 2024

Na Mohamed Ngonyani

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki katika uchaguzi muhimu wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.


Rais Samia amesema kuwa uchaguzi huo utatoa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.


Akizungumza na wananchi wakati wa hitimisho la mbio za Mwenge kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza,, Rais Samia alieleza kuwa Serikali za Mitaa ni mamlaka muhimu katika kubuni, kusimamia, na kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii kwa maendeleo jumuishi ya wananchi.




“Nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi huu muhimu. Ili tuweze kushiriki kama wagombea na wapiga kura, ni lazima kwanza tuwe tumejiandikisha,” alisema Rais Samia.


Rais Samia aliongeza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea hadi tarehe 20 Oktoba, 2024.


“Nina furaha kuwajulisha kuwa tayari nimejiandikisha katika orodha ya wapiga kura kwenye makazi yangu, kitongoji cha Sokoine, kijiji cha Chamwino Ikulu. Wananchi wote nawasihi twende kwenye maeneo yetu tukajiandikishe ili tuweze kushiriki uchaguzi wa tarehe 27 Novemba, 2024,” aliongeza Rais Samia.


Pia, Rais Samia aliendelea kueleza kuwa uchaguzi huo ni fursa kwa jamii kukuza demokrasia na maendeleo katika maeneo yetu, akinukuu msemo wa vijana, “Uchaguzi huu tusiuchukulie poa.”


“Napenda kuwakumbusha wananchi kutofautisha orodha ya wapiga kura inayotumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo hutumika wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisisitiza Rais Samia.


Mwisho alimshukuru Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kwa kufanya uzindizi wa wiki ya Vijana tarehe 11, Oktoba 2024