Thursday, October 17, 2024

 Klabu ya Pamba Jiji Fc imethibitisha kumteua kocha Fred Felix 'Minziro' kuwa Kocha Mkuu akichukua mikoba ya Goran Kopunovic aliyetupiwa virago Oktoba 16, 2024.


Taarifa ya leo Oktoba 17, 2024 iliyotolewa na Kaimu C.E.Ο kwa klabu hiyo, Ezekiel Ntibikeha imebainisha kuwa Minziro atashirikiana na Kocha msaidizi Mathias Wandiba.


“Uongozi wa Pamba Jiji Fc unawatakia kila la kheri katika kipindi hiki cha kazi yao mpya, huku wanamwanza wakiwa na matumaini kibao ya kuiona Pamba Jiji ikifanya vizuri Ligi Kuu.” — imesema taarifa hiyo.

Wednesday, October 16, 2024

 Kamanda wa Polisi Jamii Wilaya ya Kipolisi Ukonga ASP Novatus Edmund Mallya amewaasa Polisi Jamii kuacha kutumia vibaya mwamvuli huo katika kutekeleza majukumu yao pamoja na ndani ya jamii wanayoishi.



ASP Mallya ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa Wananchi ndani ya Wilaya hiyo, "Tunapata malalamiko kutoka kwa Wananchi kuwa mnafanya matukio ya ajabu na ubabe kisa tu ninyi ni Polisi Jamii, hii sio sawa acheni kukamata Watu bila kufuata utaratibu mzuri , Biashara haramu na matendo mengine yanayokinzana na sheria za nchi ninyi muwe mfano hakuna aliye juu ya sheria."



Monday, October 14, 2024

Na Mohamed Ngonyani

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki katika uchaguzi muhimu wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.


Rais Samia amesema kuwa uchaguzi huo utatoa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.


Akizungumza na wananchi wakati wa hitimisho la mbio za Mwenge kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza,, Rais Samia alieleza kuwa Serikali za Mitaa ni mamlaka muhimu katika kubuni, kusimamia, na kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii kwa maendeleo jumuishi ya wananchi.




“Nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi huu muhimu. Ili tuweze kushiriki kama wagombea na wapiga kura, ni lazima kwanza tuwe tumejiandikisha,” alisema Rais Samia.


Rais Samia aliongeza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea hadi tarehe 20 Oktoba, 2024.


“Nina furaha kuwajulisha kuwa tayari nimejiandikisha katika orodha ya wapiga kura kwenye makazi yangu, kitongoji cha Sokoine, kijiji cha Chamwino Ikulu. Wananchi wote nawasihi twende kwenye maeneo yetu tukajiandikishe ili tuweze kushiriki uchaguzi wa tarehe 27 Novemba, 2024,” aliongeza Rais Samia.


Pia, Rais Samia aliendelea kueleza kuwa uchaguzi huo ni fursa kwa jamii kukuza demokrasia na maendeleo katika maeneo yetu, akinukuu msemo wa vijana, “Uchaguzi huu tusiuchukulie poa.”


“Napenda kuwakumbusha wananchi kutofautisha orodha ya wapiga kura inayotumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo hutumika wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisisitiza Rais Samia.


Mwisho alimshukuru Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kwa kufanya uzindizi wa wiki ya Vijana tarehe 11, Oktoba 2024