Hii ni blog ambayo inakupa Taarifa na habari Zote Za Kitaifa na za kimataifa Katika Nyanja Zote za kisiasa, Uchumi, michezo na burudani..

Sunday, September 29, 2024

 WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imetoa sh milioni 38.2 ili kufungwa kwa mfumo wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dk. Samia Suluhu Hassan mkoani Ruvuma ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Shule hiyo ya kisasa yenye wanafunzi zaidi ya 540 kwa sasa ipo katika Wilaya ya Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma ilizinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 27.



Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa shule hiyo, Mkurugenzi wa wa Mipango na Utafiti REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha wakala kutekeleza miradi yake mbalimbali kwa wakati ikiwamo miradi ya nishati safi ya kupikia.

“REA tunaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali pamoja na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo na katika shule hii tumetoa sh milioni 38.2 kwa ajili ya kufungwa mifumo ya nishati safi ya kupikia tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanatumia kuni kupikia,” amesema Mhandisi Chibulunje.


Mhandisi Chibulunje amesema, REA itahakikisha shule mbalimbali zinafungwa mfumo wa nishati safi wa kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na kuongeza kuwa wakala huo umesaini mikataba ya zaidi ya Sh bilioni 50 kuhakikisha taasisi zinazolisha watu zaidi ya 300 kama magereza na kambi za jeshi zinafungiwa mifumo ya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma kutoka REA, Martha Chassama amesema wakala umejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia huku akiendelea kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia

No comments:

Post a Comment