WANACHAMA 200 WA ACT WAZALENDO WAJIUNGA CCM
Wanachama 200 wa Chama cha ACT Wazalendo, wakiwemo viongozi wa ngazi za juu kama Katibu wa Chama hicho Jimbo la Tunduru Kusini, mkoani Ruvuma Saidi Mponda, na Diwani wa Kata ya Mchoteka, Sefu Hassan Dauda, wamejiunga rasmi na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Uamuzi wao wa kuhama ACT Wazalendo na kujiunga na CCM umetokana na kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Wanachama hao wamesema kuwa Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuboresha sekta za miundombinu, afya, elimu, na uchumi kwa ujumla.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mlimgoti, wilayani Tunduru, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewapongeza wanachama hao kwa uamuzi wao wa kujiunga na CCM.
Amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye misingi ya maendeleo na akatoa wito kwa wanachama wa vyama vingine kujiunga na chama hicho ili kushirikiana katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.
Aidha, Dkt. Nchimbi ametumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu dhamira ya CCM kuendelea kusimamia maendeleo na kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na rasilimali za nchi.
Amesema kuwa Serikali inayoongozwa na CCM itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa Watanzania wote kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote, akisisitiza kuwa mshikamano wa kitaifa ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment